1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Ukraine yatumia makombora ya masafa marefu

25 Aprili 2024

Marekani inaharakisha kutuma silaha na vifaa vingine vya kivita nchini Ukraine, baada ya Rais Joe Biden kutia saini muswada uliocheleweshwa kwa muda mrefu wa kuiunga mkono nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4fB0E
Rais wa Marekani Biden akutana na Rais wa Ukraine Zelensky katika Ikulu ya White House
Rais wa Marekani Joe Biden ametia saini muswada wa kuisaidia Ukraine kijeshi.Picha: Yuri Gripas/UPI Photo/IMAGO

Uidhinishaji wa mwisho wa sheria hiyo ambayo inajumuisha dola bilioni 61 kwa Kyiv kati ya jumla ya dola bilioni 95 za ufadhili unajiri baada ya miezi kadhaa ya mabishano ya kisiasa huku vikosi vya Ukraine vikikosa silaha na kuzidiwa  katika uwanja wa vita.

Baada ya kutia saini muswada huo na kuwa sheria, Biden alisema

"Ninahakikisha usafirishaji unaanza mara moja. Katika saa chache zijazo tutaanza kutuma vifaa nchini Ukraine kwa ajili ya zana za ulinzi wa anga, silaha, mifumo ya roketi na magari ya kivita."

"Unajua, kitita hiki ni hazina sio tu kwa usalama wa Ukraine, lakini kwa usalama wa Ulaya na usalama wetu wenyewe."

Soma pia:Ujerumani, Uingereza zaahidi kuendelea kuisaidia Ukraine

Dakika chache baada ya Biden kuzungumza, Pentagon ilitangaza kifurushi cha dola bilioni 1 kwa Kyiv kwa kutumia ufadhili huo mpya, ikijumuisha zana za ulinzi wa anga, risasi, mizinga ya kurusha makombora HIMARS, silaha za kuzuia mashambulizi pamoja na magari ya kivita.

Kupitia mtandao wa kijamii Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alitoa shukurani zake, kwa rais Biden, bunge na Wamarekani akisema kwamba lazima washinde dhidi ya Putin badala ya kumtii.

Ukraine kwa mara ya kwanza imeanza kupokea makombora ya masafa marefu yaliyotolewa kwa siri na Marekani, ambayo inaarifiwa iliyatumia kulipua uwanja wa ndege wa kijeshi wa Urusi kwenye rasi ya Crimea na maeneo mengine yanayokaliwa na Urusi.

Makombora hayo mapya, ambayo Ukraine imekuwa ikiyaomba kwa muda mrefu, yanaimarisha mashambulizi ya Ukraine kutokana na uwezo wake wa kushambulia umbali wa takriban kilomita 300.

Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan, amekiri kwamba tayari walituma makombora hayo na sasa watatuma zaidi kwani sasa wanaruhusa na pesa zaidi.  

Mashambulizi yanaendelea

Vita vya Ukraine vya Urusi
Gari latekea kwa moto baada ya kushambiliwa kwa droni.Picha: Petro Andryuschenko/Telegram/AP/picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Huku haya yakijiri afisa mkuu wa Urusi katika eneo linalokaliwa la Ukraine la Zaporizhzhia amesema kwamba raia wawili wameuawa katika shambulizi la droni ya Ukraine.

Mkuu wa mkoa aliyewekwa na Urusi Evgeny Balitsky kupitia mtandao wa kijamii amesema kwamba mwanamume na mwanamke waliuawa katika shambulizi lililolenga gari la raia na kuwaacha watoto wao wadogo wanne bila ya wazazi.

Droni zinatumiwa sana na wanajeshi wa Urusi na Ukraine katika mstari wa mbele vita, Moscow na Kyiv zalaumiana kila upande kufanya hujumaunguzi, kulenga mizinga na mifumo ya makombora.

Soma pia: Moscow na Kyiv zalaumiana kila upande kufanya hujuma

Kando na hayo, Ukraine imesema kuwa imemzuia mwanajeshi wa zamani anayetuhumiwa kusaidia vikosi vya Urusi kushambulia eneo la mashariki la Kharkiv.

Idara ya Usalama ya Ukraine imemkamata mtu huyo kwa tuhuma za "kuratibu" mashambulizi katika eneo la Kharkiv, ambalo linapakana na Urusi na sasa anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka minane endapo atapatikana na hatia.

Waendesha mashtaka nchini Ukraine wamefungua maelfu ya kesi kwa madai ya ushirikiano na adui tangu vikosi vya Urusi vilipovamia nchi hiyo mnamo Februari 2022.