1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moscow na Kyiv zalaumiana kila upande kufanya hujuma

12 Aprili 2024

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema mifumo yake ya ulinzi imezima kile ilichokitaja kuwa mkururo wa majaribio ya "mashambulizi ya kigaidi" yaliyohusisha droni za Ukraine zilizoyalenga maeneo kadhaa ndani ya Urusi.

https://p.dw.com/p/4egqu
Putin na Shoigu
Rais wa Urusi Vladimir Putin akiwa na waziri wake wa ulinzi Sergei Shoigu Picha: Alexander Kazakov/Sputnik, Kremlin Pool Photo/AP/picture alliance

Taarifa ya wizara hiyo imedai droni zisizopungua nne za Ukraine zimeharibiwa kwenye mkoa wa Rostov na nyingine moja imedunguliwa ikijaribu kufanya hujuma katika mkoa wa mpakani wa Belgorod. 

Madai hayo ya Urusi yametolewa wakati Ukraine nayo imesema mashambulizi ya droni za vikosi vya Moscow yamesababisha moto mkubwa kwenye kituo kimoja cha kufua umeme kusini mwa nchi hiyo na kuharibu miundombinu mingine.

Kyiv yaidhinisha mswada wa kuwaajiri watu jeshini wakati Moscow ikiishambulia miundo mbinu ya umeme

Katika ujumbe uliotumwa kupitia mtandao wa Telegram, jeshi la Ukraine limesema mashambulzii hayo yameyalenga majimbo ya Kherson na Dnipropetrovsk. Yameripotiwa katikati mwa miito inayotolewa na viongozi wakuu wa Ukraine wanaoyataka mataifa washirika kutuma silaha zaidi nchini humo kuvisadia vikosi vyake kujilinda mbele ya ubabe wa vikosi vya Urusi.