1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yasababisha vifo vya zaidi ya watu kumi Nairobi

25 Aprili 2024

Miili ya watu wasiopungua 13 imeopolewa kutoka maeneo tofauti ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi baada mafuriko ya kutisha kulikumba taifa hilo la Afrika Mashariki.

https://p.dw.com/p/4fARn
Mvua kubwa imenyesha nchini Kenya katika siku za hivi karibuni, na kusababisha uharibifu mkubwa
Mvua kubwa imenyesha nchini Kenya katika siku za hivi karibuni, na kusababisha uharibifu mkubwaPicha: Daniel Irungu/EPA

Serikali imeunda kikosi cha dharura kushughulikia janga hilo.Wakati huohuo, idara ya polisi imeendelea na juhudi za uokozi kwa ambao nyumba zao zimefunikwa na maji. 

Kulingana na idara ya polisi, miili ya watu wasipungua 13 imepatikana maeneo tofauti tofauti ya mji  Nairobi  kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

Vifo 11 vimetokea eneo la Mathare, moja Kibera na nyengine mtaani Kayole. Ifahamike kuwa haya ni maeneo ya mitaa ya mabanda jijini Nairobi. Inahofiwa kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka japo juhudi za uokozi zinaendelea.

Maelfu wameachwa bila makaazi kwani mvua hiyo imesababisha mafuriko yaliyoathiri nyumba na baadhi ya barabara sasa hazipitiki.

Kwa mujibu wa mkuu wa polisi kaunti ya Nairobi, Adamson Bungei, vikosi vya pamoja kutoka idara mbailmbali vinashirikiana kutoa usaidizi wa kila aina. Wakaazi wa maeneo yaliyo kwenye kingo za mito wameshauriwa kuhama anasisitiza Rais William Ruto.

Mahitaji ya msaada wa haraka

Wakati huohuo, kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amebaisha kuwa wabunge wa mrengo huo wamechangisha shilingi za Kenya milioni 1 ambazo zitakabidhiwa kwa shirika la msalaba mwekundu linalohusika na juhudi za usaidizi. 

Barabara zimegeuka kuwa mito katika mji mkuu wa Kenya Nairobi
Barabara zimegeuka kuwa mito katika mji mkuu wa Kenya NairobiPicha: Getty Images/AFP/Str

Alhamisi, waziri wa usalama wa taifa Kithure Kindiki ameiamuru idara ya taifa ya polisi kusimamia operesheni za utafuataji na uokozi kwa ndege au majini kwa ushirikiano na shirika la msalaba mwekundu. Kwengineko, maporomoko ya tope yameripotiwa kutokea Narok, Kisii na Limuru na kusababisha maafa.

Zaidiya familia 50 zimehamishwa baada ya kuathiriwa na mafuriko huko Limuru kaunti ya Kiambu.Mto Athi umevunja kingo zake na kusababisha zahma katika kaunti jirani ya Machakos. Yote hayo yakiendelea, idara ya utabiri wa hali ya hewa inatahadharisha kuwa mvua bado iko njiani.